Wednesday, August 29, 2012

OKOA MAISHA YA MTOTO HUYU; ANA VIDONDA MWILINI

MTOTO Ashura Mustafa mwenye umri wa miaka minne (pichani), mkazi wa Kijiji cha Mwandege wilayani Mkurunga, Mkoa wa Pwani, yupo katika mateso makubwa kutokana na vidonda vilivyomtoka mwilini na baba yake hana uwezo wa kumgharamia matibabu.
Baba wa mtoto huyo, Mustafa Mohamed, ana haya ya kusema: “Mtoto wangu alianza kuumwa akiwa na mwaka mmoja baada ya kuzaliwa mwaka 2007. Vidonda hivi vilianza vikiwa ni malengelenge na nimehangaika naye katika hospitali nyingi mpaka nikafika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Madaktari Muhimbili walinipa barua ya kwenda CCBRT ambako wataalamu waliniambia kuwa mtoto wangu huyu ana tatizo la saratani ya ngozi, ‘stage 4’. Nikaambiwa mtu akiwa na saratani hatua hiyo, vidonda vyake huchukua muda mrefu kupona.
“Ilitakiwa afanyiwe upasuaji lakini ikabainika kuwa hana damu ya kutosha, akapewa chupa mbili za damu lakini baada ya miezi miwili akapungukiwa tena. Akaongezewa tena chupa mbili lakini kabla ya kufanyiwa upasuaji, daktari aliyekuwa akimtibu CCBRT tukaambiwa amekwenda likizo, hivyo tukarudi nyumbani ambako yupo hadi sasa.
“Mtoto wangu ana hali mbaya kwa kuwa anakaa ndani tu tena kwenye neti kukwepa vumbi na inzi, anateseka sana. Naomba msaada kutoka kwa wasamaria kwani sina kazi na kila tunapompeleka hospitali ni lazima tukodi gari. Hali aliyonayo hatuwezi kusafiri naye kwa daladala.
“Aliyeguswa na mateso ya mwanangu awasiliane nami kwa simu namba 0769517765, 0715424607,” alisema Mustafa kwa masikitiko.

BABU LOLIONDO NI TAPELI

SERIKALI imethibitisha kuwa kitendo alichokuwa akifanya babu wa Loliondo, Mchungaji Ambilikile Masapile, cha kutoa dawa ya kutibu magonjwa, ukiwemo Ukimwi aliyokuwa amedai kuwa ameoteshwa na Mungu ni cha kitapeli.
 Utafiti umebaini kwamba dawa hiyo  ya babu wa Loliondo ni feki na kwamba haina uwezo wa kutibu Ukimwi wala kisukari.
Kwa mujibu wa  Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, utafiti wa kulinganisha wagonjwa wa Ukimwi na kisukari waliokunywa dawa hiyo na wale ambao hawakunywa, umebaini kwamba hakuna utofauti wa afya ya mgonjwa.
Alisema utafiti huo unafanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMRI), ulianza Machi mwaka huu na kwamba unahusisha wagonjwa 200 wanaofuatiliwa kwa kupimwa damu, kinga ya mwili (CD4) na uzito wa mgonjwa, ambao ulifanyika tangu mgonjwa alipokunywa kikombe cha babu.
“Matokeo ya awali ya utafiti yameonyesha kuwa hakuna utofauti katika vipimo vya kimaabara pamoja na damu, CD4, uzito na ubora wa afya ya wagonjwa kati ya waliokunywa na wale ambao hawakunywa dawa ya mchungaji,” alisema Dk. Mwinyi.

Monday, August 27, 2012

YALIYOJIRI SERENGETI FIESTA 2012 NDANI YA UWANJA WA MKWAKWANI MKOANI TANGA.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Halima Dendego pichani kati mwenye kipaza sauti akisoma namba za washindi waliojinyakulia piki piki mbili zilizotolewa na kampuni ya Push Mobile,wa tatu kulia ni Meneja Masoko wa kampuni ya Push Mobile,Rugambo Rodney na mwisho kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Clouds Media Group,Joseph Kusaga,na nyuma kabisa ni Mkurugenzi wa utafiti Clouds Media Group,Ruge Mutahaba pamoja na Mkurugenzi wa Masoko wa kampuni ya bia ya Serengeti,Ephrahim Mafuru wakishuhudia tukio hilo usiku huu kwenye uwanja wa Mkwakwani ambako tamasha la Serengeti Fiesta 2012 linafanyika.
Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Halima Dendego akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Clouds Media Group,Joseph Kusaga usiku huu mara baada ya kuwataja washindi waliojishindia piki piki mara baada ya kuchezeshwa bahati nasibu,wakati tamasha la Serengeti Fiesta 2012 likiendelea,pichani kati ni Afisa Mahusiano wa Clouds Media Group, Simon Simalenga.
Msanii wa muziki wa kizazi kipya Nuru akitumbuiza jukwaani usiku huu na shabiki wake mbele ya wakazi wa jiji la Tanga wanaondelea kutiririka ndani ya uwanja wa Mkwakwani ambako tamasha la Serengeti Fiesta 2012 linafanyika.
Msanii kutoka THT,ajae kwa kasi katika anga ya muziki wa bongofleva aitwaye Rachel akiimba jukwaani usiku huu.

AJIFUNGUA MTOTO MWENYE VICHWA VIWILI

Mwanamke mmoja nchini India amejifungua mtoto wa kike  mwenye vichwa viwili na miguu zaidi ya miwili katikaka tukio lililotokea katika jimbo la Uttar Pradesh katika hospitali ya Aashirwad .Mtoto huyo ana  vichwa viwili kwenye shingo moja na anatumia midomo yote miwili kulia..
  Daktari wa hospitali alipojifungulia mwanmke huyo anasema hali hiyo isiyo ya kawaida iantokea mara moja kwa watoto wengi wanaozalia na husababishwa na genetic disorder.
 Baba wa mtoto huyo Tilakdhari Yaday anasema huo ulikuwa uzao wao wa sita kwa yeye na mkewe huyo.

MAWAZO HUCHANGIA UGUMBA KWA WANAWAKE

 
TAFITI umebaini kuwa wanawake wengi wenye viungo salama lakini hawazai, wana kiasi kikubwa cha homoni ya Cortisol inayoletwa na uchovu.
Aina hii ya homoni ndiyo inayosimamisha mchakato wa uzalishaji wa mayai kwa wanawake wanaoshiriki mchezo wa riadha.
 Hivyo basi, uwiano huu wa kasoro za ukuzaji mayai kati ya wakimbia riadha na wanawake wagumba unaweka usawa baina ya uchovu mkubwa wa mazoezi ya viungo na ule uchovu unaotokana na msongo wa mawazo ya ugumba.
Ukweli pekee ambao nimeukusudia kuuzungumza leo ni kuhusiana na wanawake wasiokuwa na matatizo ya uzazi ambao utafiti  ulioandikwa katika jarida la Minerva Ginecologica la nchini Italia unaonesha mawazo ndiyo unaochangia kwa kiasi kikubwa wanawake hao wasipate watoto licha ya kwamba kibaiolojia hawana matatizo.
Imebainika kuwa, wanawake wengi hujisogeza wenyewe katika nguvu ya kukosa watoto kutokana na ukubwa wa kiu yao ya kupata watoto hao.
Hawa hujiweka katika uzalishaji mkubwa wa homoni ya Cortisol ambayo huchipuka kwa kasi kutokana na msukumo wa kiu kubwa na ya haraka ya kutaka kukumbatia mwana.
Kutokana na ukubwa wa tatizo hili, imebainika kuwa wagumba wengi wasiokuwa na kasoro katika viungo vyao vya uzazi wanaweza kupona au kupata watoto bila hata kupewa tiba ya miti shamba au vidonge. Tiba kubwa iliyobainishwa ni kupatiwa nasaha zitakazowaondolea mawazo tasa, wasiwasi na kutojiamini.

(CHADEMA) kumchukulia hatua za kisheria Nape Nnauye


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Nape Nnauye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM kufuatia madai ya uzushi na uongo
aliyoyatoa tarehe 12 Agosti 2012 kuwa anao ushahidi kwamba CHADEMA kimekuwa kikiwahadaa wananchi kwa kuwachangisha fedha huku kikipokea mabilioni ya fedha kutoka kwa wafadhili kutoka nje.


Izingatiwe kuwa matamshi yake yalitangazwa na vyombo vya habari vya kielekroniki ikiwemo vituo vya televisheni, radio na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii tarehe 12 Agosti 2012 na katika kurasa za mbele za magazeti mbalimbali tarehe 13 Agosti 2012.

 
Bodi ya Wadhamini wa CHADEMA iliagiza wanasheria wamwandikie barua ya kumtaka kukiomba radhi Chama Cha Demokrasia na Maendeleo kwa kutumia njia ile ile aliyotumia kufanya propaganda chafu za kuikashifu na kuifitisha CHADEMA kwa umma wa watanzania ikiwemo kuzusha kuwa upo uwezekano wa CHADEMA kupewa fedha hizo kwa mikataba yenye masharti ya kuiweka nchi rehani.

RAY C ATUA BONGO, ASAKA MUME

MSANII ‘first class’ wa muziki wa kizazi kipya Bongo, Rehema Chalamila ‘Ray C’, amerejea Bongo na kutangaza kusaka mume huku akiweka wazi vigezo anavyotaka awe navyo, Jelard Lucas anashuka nayo.
Akichonga na Over The Weekend juzikati, Ray C aliyekuwa amejichimbia nchini Kenya, alisema mwanaume atakayeweza kupata penzi lake anatakiwa kuwa na elimu ya kawaida, maendeleo, asiwe mwanamuziki wala pedeshee, awe na mvuto na mwenye kuyajua vizuri malavidavi.
Mwanadada huyo ‘chakaramu’ aliongeza kuwa mwenye sifa hizo akipatikana, atamzalia watoto wawili na kujenga naye familia bora kwani amechoshwa na maisha ya usela.
“Sina mume wala mpenzi, kwa sasa nipo single, ukiniulizia ishu za zamani ntakushangaa kweli, vigezo ndiyo hivyo, kama kuna mtu yupo tayari ajitokeze tufunge ndoa,” alisema Ray C.
Kuhusu kurudi kwenye gemu, Ray C aliwaahidi mashabiki zake kuwa baada ya mfungo kumalizika, yupo kwenye harakati za kuzindua albamu yake mpya aliyoipa jina la ‘Moyo Waniuma’ yenye nyimbo 10.
Aliongeza kuwa soko la muziki Bongo ni bovu sana ukilinganisha na Kenya hivyo bado mishemishe zake nyingi atakuwa akizifanyia nchini humo