Wednesday, August 1, 2012

AVIMBA MGUU, AENDA KUOMBEWA

 Hujafa hujaumbika, ni kauli iliyotolewa mama aliyejitambulisha kwa jina la Jacqueline Chema ambaye alikutwa hivi karibuni na chanzo chetu katika Kanisa Kuu la Huduma ya Maombezi linaloongozwa na Nabii Flora Peter lililoko Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.
Jacqueline au Jack, mama mwenye mtoto mmoja alisema tatizo alilonalo lilimuanza mwaka 2004 na kuanza kutafuta msaada katika hospitali mbalimbali ikiwemo ya magonjwa ya saratani, Ocean Road ya jijini Dar es Salaam.
Jack alikuwa na haya ya kusema: “Nimehangaika sana baada ya kuanza kuugua mguu huu mwaka 2004. Nilianza kuumwa homa kali mara kwa mara baadaye ukaanza kuvimba hapa (akaonesha mguu). Sielewi nini kimesababisha tatizo hili.
“Nimekwenda katika hospitali nyingi kupata tiba na nikafika Ocean Road lakini sijapona. Nikaamua kuja kufanyiwa maombi katika kanisa hili. “Kuumwa kwangu kumeniharibia ratiba zote za maisha yangu. Siwezi kufanya kazi yoyote na hata kuzaa.

“Siwezi kuzaa nikiwa katika hali hii japokuwa nina mume. Nimehangaika sana na kwa kuwa hospitali waliniambia sina kansa, nimekata tamaa kimatibabu na sasa nategemea maombezi.
“Nawaomba Watanzania waniombee ili nipone na kuondokana na tatizo hili. Sina cha kufanya, yeyote atakayetaka kunisaidia kwa njia yoyote nitashukuru. Nilikuwa nashindwa kutembea lakini tangu nimeanza kuombewa hapa kwa Nabii Flora, naweza kutembea japokuwa kwa shida. Naamini nikizidisha maombi, nitapona kabisa.”
Kwa upande wake Nabii Flora alisema kwa uwezo wa Mungu Jack atapona ndani ya siku 21 kwani hakuna kitu kinachoshindikana mbele yake.
Mama huyu anaumwa, hawezi kufanya chochote cha kujiingizia kipato, yeyote aliyeguswa na habari hii na kutaka kumsaidia kwa hali na mali anaweza kumpata kwa simu namba 0654 136270- Mhariri.

No comments:

Post a Comment