KUMEZUKA vitendo vya unyama mkoani Mbeya vya kuzika watu wanaotuhumiwa
kuwa ni washirikina wakiwa hai ambapo hivi karibuni watu wawili akiwemo
mwanamke mmoja wamefanyiwa unyama huo.
Mwanamke aliyezikwa akiwa hai
kwa tuhuma za kujihusisha na ushirikina ni Rozina Mwadala (60) ambapo
tukio hilo lilitokea Juni 2, mwaka huu.
Mwanamke huyo alichukuliwa
hatua hiyo baada ya kifo cha mmoja wa ndugu yake ambaye alifariki muda
mchache baada ya kulalamika kuwa alikuwa akiumwa sikio na kichwa. Hata
hivyo, hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa tayari kuhojiwa na mwandishi
wetu kwa hofu ya kukamatwa na polisi.
Kufuatia vitendo hivyo kushika
kasi mkoani Mbeya, Mwenyekiti wa Muungano wa Jamii Tanzania (Mujata),
Chifu Soja Masoko, amewaonya wananchi wa Kijiji cha Malamba, Wilaya ya
Mbarali mkoani Mbeya kuacha mara moja tabia za kujichukulia sheria
mikononi alipokuwa akiwahutubia katika mkutano wa hadhara Juni 15, mwaka
huu.
“Hasara yake mnaona. Sasa kufuatia kitendo hicho cha
kikatili baadhi ya wananchi wamehama kijijini hapa kukwepa mkono wa
sheria na shughuli za kiuchumi zimezorota,” alisema.
Mbali na
mwanamke huyo kuzikwa hai, hivi karibuni mwanaume mmoja, Nyerere Kombwee
naye alizikwa hai baada ya kutokea kifo cha mdogo wake kisha yeye
kutohudhuria msibani ndipo wananchi wakamsaka na walipompata wakampiga
na yeye akatoa vitisho kuwa damu yake isingeweza kwenda bure ndipo
wakaamua kumzika akiwa hai.
No comments:
Post a Comment