Tuesday, July 10, 2012

Kigogo anataka kuwaua baadhi ya wabunge wa chadema



MBOWE ASEMA MPANGO HUO UNARATIBIWA NA KIGOGO WA USALAMA WA TAIFA, MKUCHIKA ASEMA NI TUHUMA NZITO, AZIVUTIA KASI
 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),kimetoa tuhuma nzito kikidai kigogo mmoja (jina tunalo) wa Idara ya Usalama wa Taifa anaratibu mpango wa kuwaua viongozi wake waandamizi akiwamo Katibu Mkuu, Dk Willbrod Slaa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.
Kwa sababu hiyo, chama hicho kimeitisha kikao cha Kamati Kuu (CC) leo kujadili mambo mbalimbali na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe amesema ajenda kuu itakuwa kuzungumzia usalama wa viongozi wao kutokana na vitisho hivyo.
Kuhusu tuhuma hizo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika amesema tuhuma hizo ni nzito na atazijibu kwa maandishi.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam jana, Mbowe alitaja majina ya baadhi ya maafisa idara hiyo (majina tunayahifadhi) na kudai kuwa mmoja kati yao ndiye anayeratibu shughuli hiyo na tayari yupo mjini Dodoma kwa ajili ya kuongoza  kundi linalotaka kumdhuru Mnyika.
 
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alisema mbali na viongozi hao wawili, mwingine aliyedai kuwa anafuatiliwa ni Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema akidai kwamba, taarifa zinaonyesha kuwa wanafuatiliwa kwa saa 24.
Mbowe alidai kwamba idara hiyo ambayo haifanyi shughuli za siasa, inatumia ofisi yake vibaya kwa kufuatilia viongozi hao wakidhani chama hicho kina mambo ya siri kinayotaka kuyafanya katika nchi hii.
 
“Sisi Chadema hatuna mambo ya siri tunayotaka kufanya katika nchi hii. Matatizo ya Watanzania yapo wazi na yanajulikana na kila mmoja, Serikali ya CCM itekeleze sera na ahadi zao kwa wananchi na si vitisho,” alisema Mbowe na kuongeza:
 
“Tunaomba wananchi waelewe kuwa viongozi wao wako hatarini, lakini Chadema hatutarudi nyuma katika kutetea haki  za wanyonge hata kwa kufa na hatuwezi kupeleka malalamiko yetu polisi sababu nao ni sehemu ya tatizo.”
 
Alisema chama chake kimekuwa kikihusishwa na mambo mengi ukiwamo mgomo wa madaktari unaoendelea na kusema Chadema hakiko nyuma ya mgomo huo na hakijawahi kukutana na kufanya kikao na madaktari.
 
“Wametuhusisha na mambo mengi na sasa wanasema tuko nyuma ya mgomo wa madaktari, taarifa hizo siyo za kweli na wala hatujawahi kukaa nao kikao chochote kujadili masuala yao, madaktari wana madai ya haki zao. Hapa tunaingia kwenye utaratibu wa kutesana ili kupata taarifa, mmesikia Dk Ulimboka aliteswa ili aseme Chadema iko nyuma ya mgomo,” alidai Mbowe.
 
Hata hivyo, Mbowe alisema suala la kutokuwa nyuma ya mgomo huo haliwanyimi fursa ya kutetea makundi ya watu wanaodai haki zao wakimwamo madaktari na kusema anaunga mkono tamko la viongozi wa dini.
 
“Viongozi wa dini wametoa tamko lao jana (juzi), wakitaka Serikali kuwarudisha madaktari na kumalizia suala hilo kwa njia ya mazungumzo,” alisema.
Alisema Chadema kinaunga mkono tamko hilo akisema si busara kuwa fukuza kwa sababu Serikali imetumia gharama kuwaandaa.
Dk Slaa anena
 
Kwa upande wake, Dk Slaa alisema Chadema kimeamua kutotoa madai yake polisi akidai kuwa imepokea madai mengi kutoka kwa viongozi na wanachama ya kutendewa visivyo lakini hakuna hata moja lililowahi kufanyiwa kazi.
Kuhusu kitisho la kuuawa alidai kwamba alianza kutishiwa siku nyingi na kusisitiza kuwa hilo haliwezi kuwanyamazisha.
 
“Taarifa za sasa wanaanza na Mnyika na kufuatia mimi, ninachosema wafanye watakavyo hatutaacha kufanya kazi yetu, hata nilipoibua tuhuma za EPA niliwaambia watuhumiwa wengine wa sakata hilo ni Usalama wa Taifa,” alisema Dk Slaa.
 
Dk Slaa alitaja baadhi ya mambo ambayo alidai kuwa hayakushughulikiwa yalipowasilishwa polisi kuwa ni vinasa sauti alivyowekewa kwenye chumba alichokuwa amelala wakati wa vikao vya Bunge Mjini Dodoma.
Alisema vifaa hivyo vilichukuliwa na polisi kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi lakini hadi leo hakuna taarifa iliyotolewa hata kwake licha ya kuwa mhusika mkuu.
Mnyika: Namwachia Mungu
 
Akizungumzia madai hayo, Mnyika alisema anamuachia Mungu kwa kuwa ndiye aliyetoa uhai hata kwa hao wanaofikiria kutekeleza kitendo hicho.
Mnyika alidai kuwa baada ya kupata taarifa hizo ambazo alisema zimeandaliwa kwa ama kunyeshwa sumu au kuvamiwa na majambazi, alikutana na familia yake na uongozi wa chama chake ambao kwa pamoja wamemtaka aendelee na kazi ya kutetea rasilimali za taifa.
 
“Nilipopata taarifa hizi nimekutana na viongozi wangu wa chama na jana usiku (juzi), nilikutana na familia yangu, kwa pamoja wameniambia niendelee na kazi hii ninayoifanya kwani nimetumwa na wananchi na sauti ya wengi ni sauti ya Mungu, ”alisema Mnyika.
Kwa upande wake, Lema alisema  taarifa za kufuatiliwa na watu hao wanaodaiwa kuwa ni wa Usalama wa Taifa alizipata kwa mmoja wa vyanzo vyake kutoka serikalini.
 
“Nilipigiwa simu na mtu mmoja kutoka serikalini aliyeniambia kuna gari nyuma linanifuatilia, nilipogeuka niliona na kusimama kisha nikashuka na kubadili gari na lenyewe likaendelea kunifuatilia katika gari nililokuwa nimepanda,” alidai  Lema.

Lema alidai kwamba hata juzi asubuhi alikutana nalo katika nyumba aliyofikia na alipolikaribia watu hao walishusha vioo na kumsalimu wakimwita ni Mbunge wa Arusha aliyeko kwenye likizo.

No comments:

Post a Comment