NI safari ya siku mbili kutoka mjini Songea makao makuu ya mkoa
wa Ruvuma hadi kuweza kuifikia shule ya msingi Ndonga iliyopo wilayani
Nyasa mwambao mwa ziwa Nyasa.
Basi linaishia katika mji mdogo wa Liuli, Ziwa Nyasa na kutoka hapo
inakulazimu kukodi pikipiki hadi katika kijiji cha Njambe kata ya
Kihagara ambapo ndiyo mwisho wa usafiri wa pikipiki na kuanzia hapo
inakulazimu kutembea kwa miguu kwa takribani saa moja hadi kukifikia
kijiji cha Ndonga!
Shule ya msingi Ndonga imejengwa juu ya mlima wa Liwundi, unapofika
katika kijiji cha Ndonga inakulazimu kupanda mlima wenye mwinuko mkali
wenye makorongo kwa takriban zaidi ya saa moja hadi kufika kileleni
ndipo unakutana na shule hii.
Asilimia 90 ya wanafunzi wanaosoma katika shule ya msingi Ndonga
wanaishi chini ya mlima hivyo inawalazimu kwa siku tano yaani Jumatatu
hadi Ijumaa kupanda na kushuka mlima kwa saa mbili hali ambayo
imesababisha shule hiyo kukabiliwa na utoro uliokithiri wa wanafunzi
ambao unafikia kwa siku kati ya asilimia 60 hadi 70.
Akizungumza kwa niaba ya mwalimu mkuu, mtaaluma wa shule ya msingi
Ndonga Amos Kilongo anasema shule hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi
ambazo zinachangia kushusha taaluma kwa wanafunzi mwaka hadi mwaka na
kwamba hakuna juhudi zozote zinazofanywa na serikali ya kijiji wala
ngazi ya wilaya kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo.
“Nakupongeza sana kwa kuweza kupanda mlima wenye muinuko mkali na
kufika hapa shuleni, hatujawahi kupokea wageni kutoka ngazi ya wilaya
tangu shule hii ilipoanzishwa mwaka 1995, shule haijawahi kukaguliwa
tangu mwaka 1995 ilipokaguliwa wakati inaanzishwa’’, alisisitiza.
Sera ya elimu inaeleza wazi kuwa kila shule ya msingi inatakiwa
angalau ikaguliwe kila mwaka kwa lengo la wakaguzi kuwakumbusha walimu
na kutoa mwongozo wa ufundishaji wenye tija na uendeshaji wa shule
kulingana na maelekezo ya wizara ya elimu.
Kulingana na mwalimu wa shule ya Ndonga, shule hiyo yenye wanafunzi
309 wanaosoma kuanzia darasa la awali hadi la saba inakabiliwa na
upungufu mkubwa wa vyumba vya kusomea hali inayosababisha darasa la
awali lenye wanafunzi 37 kusomea chini ya mti.
Anabainisha kuwa shule hiyo ina vyumba vinne tu vya madarasa hali
ambayo imesababisha madarasa mawili kusomea katika chumba kimoja na
kwamba kuna madarasa mawili ambayo yameezuliwa na upepo kwa zaidi ya
mwaka mmoja hayajaezekwa hali ambayo inasababisha wanafunzi kusomea huku
wakipigwa na jua na mvua.
“Mazingira duni ya kujifunzia yaliopo katika shule hii yamesababisha
utoro wa wanafunzi kufikia kati ya asilimia 60 hadi 70 kwa siku,walimu
tunafanyakazi katika mazingira magumu, shule ina nyumba moja tu ya
mwalimu mkuu yenye vyumba vitatu ambayo tunaishi walimu watatu na
familia zetu, mimi nimeamua kuishi jikoni kwa kuwa mwalimu mkuu ana
familia kubwa hali ni mbaya’’, alisema kwa uchungu.
Mwalimu wa taaluma katika shule hiyo Amos Kilongo anasema hali ni
mbaya kutokana na mazingira duni yaliyopo katika shule hiyo ambapo
takwimu za ufaulu kuanzia mwaka 2007 hadi 2011 zinathibitisha kiwango
cha ufaulu kuwa chini ambapo shule hiyo hivi sasa ina wanafunzi 50
wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Mwaka 2011 wanafunzi waliohitimu darasa la saba katika shule hiyo
walikuwa ni 29 waliofaulu ni wanafunzi watano (5) kati yao wavulana ni
wanne na msichana mmoja, mwaka 2010 waliohitimu walikuwa ni 24,
waliofaulu ni wavulana wawili tu, mwaka 2009 waliohitimu walikuwa
wanafunzi 32, waliofaulu ni wanane kati yao wavulana watano na wasichana
watatu, mwaka 2008 waliohitimu walikuwa 60 waliofaulu 48 kati yao
wavulana 22 na wasichana 26.
Hata hivyo anabainisha kuwa mwaka 2007 katika shule hiyo hapakuwepo
na wanafunzi wa darasa la saba kutokana na wanafunzi wachache waliofaulu
darasa la nne ambao waliunganishwa na darasa la tatu hivyo kuwa
wanafunzi 60 waliohitimu mwaka 2008.
“Kutokana na mazingira duni ya shule hiyo ikiwemo kijiji kukosa
barabara ya kuweza kupita gari, kila mwaka wakati wa mitihani ya Taifa
ya darasa la saba shule hiyo imepewa masafa (route) maalum ambapo gari
la mitihani linaishia katika kijiji cha Njambe na baada ya hapo mkuu wa
msafara mlinzi pamoja na msimamzi wanabeba mitihani kichwani na
kutembea kwa zaidi ya kilometa saba hadi juu la mlima ambapo ipo shule
hii’’, alisema.
Walimu watano wote wanaume wanaofundisha katika shule hii wakiwemo
Gorge Mbapira, Joel Makelele, Amos Kilongo Edward Msuya na Atanas
Mhagama wamekata tamaa kuendelea kufundisha katika mazingira duni ambayo
yanawakosesha huduma zote muhimu ikiwemo mawasiliano, afya, usafiri,
maduka na huduma zote muhimu.
Mratibu elimu kata ya Kihagara Severine Ngwenya anasema shule ya
Ndonga licha ya kupewa fedha za mpango wa uboreshaji wa elimu ya msingi
MMEM mwaka 2002 hadi 2005 bado mazingira ya shule hiyo ni duni kwa kuwa
hakuna chumba hata kimoja cha darasa ambacho kimepigwa sakafu badala
yake wanafunzi wanasomea kwenye vumbi.
“Hali ya shule ya Ndonga kwa ujumla wake ni mbaya na haifai kwa
kufundishia na kujifunzia, shule haifikiki kwa gari wala pikipiki bali
kwa mguu unapanda mlima kwa saa mbili, hata wilayani hawajawahi kufika
katika shule hiyo’’, alisema.
Edward Ndunguru afisa mtendaji wa kijiji cha Ndonga anaitaja mikakati
ambayo inachukuliwa hivi sasa na kijiji hicho ni kufyatua tofali
200,000 hata hivyo tofali zilizofyatuliwa ni 60,000 ambazo zitatumika
kwa ajili ya kuongeza vyumba vya madarasa na nyumba za walimu katika
shule hiyo.
Mbunge wa jimbo la Mbinga mashariki Kapt. John Komba ambaye shule
hiyo ipo katika jimbo lake amekiri kijiji cha Ndonga kuwa ni miongoni
mwa vijiji ambavyo vinamsumbua kichwa, hata hivyo amesema yupo tayari
kusaidia kutoa vifaa vyote vya ujenzi wa shule hiyo iwapo wananchi
watakubali kuihamisha shule kutoka mlimani na kuijenga eneo
linalofikika kirahisi.
Afisa elimu msingi katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga David Mkali
ambaye anawajibika katika wilaya ya Nyasa amesema ameandaa takwimu za
mapungufu mbalimbali yaliyojitokeza katika shule za msingi ikiwa ni
pamoja na upungufu wa vyumba vya madarasa, madawati, walimu na nyumba za
walimu kisha kuweka mpango mkakati wa kukabiliana na matatizo hayo.
“Natambua changamoto zinazoikabili shule ya msingi Ndonga,
kijiografia shule hiyo haifikiki hali ambayo inasababisha wakaguzi
kushindwa kwenda kuikagua kila mwaka hata wakati wa mitihani inakuwa na
route maalum, shule kuihamisha toka mlimani ni gharama kubwa sio jambo
rahisi inawezekana ukawa mpango wa muda mrefu’’, alisema Afisa elimu.
Afisa elimu huyo ameitaja mikakati mingine ya kuinua kiwango cha
ufaulu kuwa ni kuzitembelea shule za msingi kwa kushirikiana na idara ya
ukaguzi wa shule ili kufuatilia utendaji kazi wa walimu na kusikiliza
changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.
No comments:
Post a Comment