Mabilioni ya Uswisi – Tusigeuzwe Mazezeta
Jumanne tarehe 20 Novemba 2012,
baadhi ya vyombo vya habari vimebeba habari zinazohusu matamshi ya
Waziri wa Utawala Bora ndugu George Mkuchika kuhusu sakata ya mabilioni
ya Uswisi. Waziri amesema kwamba Serikali ya Uswisi inataka majina ya
Watanzania walioficha fedha huko ndio waweze kusaidia uchunguzi. Habari
kama Hiyo, yenye maudhui na malengo hayo hayo iliandikwa na Gazeti la
The Guardian on Sunday la tarehe 18 Novemba 2012.
Nimeona ni vema nitoe kauli
yangu rasmi kuhusu suala hili. Lengo ni kuweka rekodi sawa juu ya Azimio
la Bunge na kwamba Serikali inapaswa kutekeleza Azimio na sio kutoa
kauli tata za kukata tamaa.
Moja, Suala hili japo sio jipya
lakini limeandikwa kama ni jambo jipya. Suala la Serikali ya Uswisi
kutaka majina lilisemwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati
akichangia hoja binafsi niliyowasilisha Bungeni na pia wakati akileta
maombi yake ya kuiondoa hoja ambayo yalikataliwa na Bunge. Kama sio
sababu mpya ni kwanini imeibuka upya na kwa kasi? Ni wazi Serikali
inajihami kwa kuona kuwa itashindwa kutekeleza azimio la Bunge.
Watanzania wasikubali propaganda hii ya Serikali. Bunge limeagiza
Serikali kufanya uchunguzi kwa kutumia njia za kiserikali au wachunguzi
binafsi wa kimataifa. Kwa nini Serikali inaanza kubwabwaja ilhali wala
haijaanza kazi hiyo? Serikali inajaribu kuficha nini? Kwa nini baada ya
wiki iliyopita Benki Kuu kufanya uchunguzi kwenye Mabenki ya Biashara
jijini Dar es Salaam na namna fedha zimekuwa zikipelekwa nje
(international transfers), leo Serikali inakuja na kauli za kukakata
tamaa? Kunani?
Pili, Watanzania wajue kwamba
Taifa la Swiss limejengwa na linajengwa kwa fedha hizi za wizi ambazo
watu mbalimbali duniani wanaiba au kukwepa kodi kwenye nchi zao na
kuzificha huko. Serikali ya Swiss hata siku moja haiwezi kutoa
ushirikiano kwa Serikali ya Tanzania katika suala kama hili. Ndio maana
Azimio la Bunge linataka wachunguzi binafsi ambao hawatahitaji
ushirikiano wa Serikali ya Swiss. Nawakumbusha kwamba mwaka 1997 mara
baada ya Joseph Desire Mobutu kuangushwa na Rais Joseph Kabila kule
Kongo – Kinshasa, Serikali ya Swiss iliitaka Serikali ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo kuonyesha ushahidi kuwa hela hizo za Mobutu
zilikuwa zimepatikana kwa njia haramu! Waswiss walitaka Kabila
awakakikishie kuwa fedha zile zaidi ya dola bilioni nane za Kimarekani
Mobutu hakuzipata kihalali ndio waweze kuzirejesha. Zaire ilikadiriwa
kuwa na zaidi ya dola za Kimarekani bilioni thelathini katika Mabenki ya
nje ya nchi hiyo. Majibu ya aina aina hii ni majibu ‘standard’ ambayo
kila nchi inapewa. Hata Marekani ilipokuwa inafuatilia wakwepa kodi wao
walijibiwa hivi hivi. Hatimaye Serikali ya Marekani ikaamua kununua
taarifa hizo na kuwakamata wakwepaji kodi wao walioficha fedha Uswisi.
Hao ndio Waswiss ambao Serikali ya Tanzania inashabikia majibu yao. Bila
Aibu Mawaziri wetu wanayanukuu majibu ya Waswiss kama kasuku. Tunasahau
historia haraka sana. Tunakuwa kama mazezeta.
Tusiwe Taifa la mazezeta.
Mabwege na mazezeta huimba kila wanachoambiwa kuimba. Sasa Serikali ya
Tanzania imekuwa msemaji wa Serikali ya Swiss badala ya kuchunguza
utoroshaji wa fedha haramu na kisha kutoa taarifa Bungeni. Naitaka
Serikali ianze uchunguzi mara moja kama namna ilivyoelekezwa na Bunge.
Suala hili sio suala la kisiasa, sasa ni Azimio la Bunge ambalo
linahitaji kutekelezwa kikamilifu. Suala hili sio suala la Zitto Kabwe
tena, ni suala la Bunge, ni suala la Wananchi. Wananchi hawataki uzezeta
wa watu waliopewa dhamana ya kutekeleza Azimio lao. Kama hawawezi
wapishe watu wenye uwezo wa kusimamia maslahi ya Watanzania kwa kuchukua
hatua stahili za kuchunguza utoroshaji mkubwa wa fedha za kigeni,
ukwepaji mkubwa wa kodi na ufisadi uliopelekea Watanzania kuficha
mabilioni kwenye mabenki nje ya Tanzania. Hatutakaa kimya mpaka tuone
mwisho kamilifu wa suala hili. Utekelezaji wa Azimio la Bunge itakuwa ni
salamu tosha mafisadi na watoroshaji wa fedha haramu kwamba hawana pa
kujificha na Tanzania sio Taifa la kuchezeachezea. Lazima tushinde vita
hii. Anayeona hawezi kutuongoza kuishinda atupishe mapema. Hatupaswi
kuwa Taifa la Mazezeta. Watanzania sio mabwege tena, Mwakyembe alipata
kusema.
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Kigoma Kaskazini.
No comments:
Post a Comment