KWA sehemu kubwa, maisha ya mwanadamu yanategemea sana ushirikiano wa
watu wenzake. Watalaamu wanasema mafanikio na kutofanikiwa ni watu.
Huwezi kusema umefanikiwa kisiwani kusikokuwa na watu ambao watakuwa
sehemu ya mafanikio yako. Mtu yeyote hataonekana ameendelea kwa kuwa na
viwanda vingi msituni wanakoishi wanyama wasiofahamu umuhimu wa nyama ya
kusindika.
Aidha, kipimo cha kutofanikiwa hakitokani na maisha ya
upweke bali ya kujilinganisha na watu wengine wanaozunguka maisha yako
ya kila siku. Tajiri wa kijijini ni yule anayemiliki Bajaj ambazo
wengine kwenye eneo analoishi hawana.
Ni ukweli ulio wazi kwamba
utajiri wa mtu wa shamba wanakoishi maskini wengi hauwezi kuwanyima
usingizi matajiri wa mjini wanaotembelea magari na kuishi kwenye nyumba
za kifahari. Maana yangu hapa ni kwamba maisha ni watu.
Siku zote
kwenye maisha yangu ninapokutana na binadamu wenzangu huwafikiria katika
sehemu mbili. Kwanza kukwama kokote katika maisha kutatokana nao,
lakini pili, ni kufanikiwa kwangu sehemu ya ninachokitarajia kutoka
kwao.
Ufahamu huu umenisadia sana. Kila mara niwapo na rafiki zangu
huwatazama katika sura hizo mbili kwamba nifanikiwe au nisifanikiwe kwa
ajili yao.
Nimetafakari na kuamini kuwa somo la aina mbili za watu
wanaoweza kukukatisha tamaa kwenye maisha yako linaweza kukusaidia,
msomaji wangu, kufikia ujuzi wa elimu ya jinsi ya kufahamu namna
binadamu wenzako wanavyoweza kukuletea mafanikio au kutofanikiwa.
Bila shaka katika maisha yako umekutana na watu ambao walikukataza
usifanye jambo fulani ambalo wewe uliamini kabisa lingekusaidia kufikia
mafanikio uliyokusudia kwenye maisha yako.
Sikia kauli hii: “Jambo
unalotaka kufanya haliwezi kufanikiwa, unajisumbua bure.” Yawezekana
ulishaambiwa hivi na ukaogopa, ukasita, ukakata tamaa ya kuanzisha
biashara kwa sababu rafiki, wazazi au ndugu zako wamekuambia hutaweza
kufanikiwa.
Naomba ujifunze kwamba, watu ambao ni hodari kwa kauli
za aina hii ni wale wanaotoka katika makundi mawili hatari. KWANZA ni
wale wanaoogopa kujaribu kufanya jambo. PILI ni wale ambao hawapendi
kukuona unafanikiwa kwenye maisha yako.
Mtu ambaye ni mwoga wa
kujaribu, usitegemee hata siku moja atakumbia “fanya”. Anachojua yeye
ni kueneza woga wake. “Bwana usiende kubeba zege utapata matatizo ya
kiafya, usifanye hiki na kile kuna hili na lile,” hizo ni baadhi ya
kauli atakazokuambia.
Hivyo, kuwa makini na watu waoga wa kujaribu, usiwape nafasi ya kukukatisha tamaa, hutafanikiwa kamwe!
Kundi la pili la kuwa nalo makini ni la wale ambao wanaogopa
utafanikiwa. Watu ambao wanahofia uwezo wako utakufanya ufanikiwe na
kuwashinda kwenye eneo hili na lile, watakupiga vita vya maneno ili
kukukatisha tamaa, ubaki kama wao ambao hawakujaliwa uwezo ulio nao.
Puuza kauli za watu wasiopenda ufanikiwe, hata wakikuambia kuwa kusoma
kwako hakutakusaidia waambie: “Kama ninyi mmesoma na hamkufanikiwa, ni
ninyi lakini mimi mafanikio yangu ni elimu.”
Asante kwa kunisoma, tukutane tena wiki ijayo kwa somo lingine zuri zaidi.
No comments:
Post a Comment