Monday, October 22, 2012

Umetendwa? Futa machozi, tazama mbele, usijilaumu wala usijute

 
Busara, hekima na moyo imara ni vipengele vikuu vitakavyokuwezesha kuvuka changamoto mbalimbali kwenye mapenzi. Fikiria kwamba hata barabara iliyochongwa vema na wahandisi waliobobea, bado milima na mabonde vitakuwepo.
Kama ndivyo, basi inashindikana vipi kutokea kwa hali isiyoeleweka kwenye mapenzi? Ni mambo ya kawaida mno, kwa hiyo busara na hekima viwe ndani yako. Vilevile moyo imara ukupe nguvu ya kuvuka changamoto za hapa na pale.

 
Unatakiwa uwe mwepesi kukubali matokeo. Inapotokea umejikuta upo kwenye uhusiano na mtu mbaya, basi ikupe sababu ya kuona kwamba ni bahati kukutana naye ili akupe elimu ya uhusiano. Utajuaje kasoro za kimapenzi kwa mtu wa ovyo ikiwa hujakutana naye?
Hapa simaanishi kwamba watu wawe wanajaribu mapenzi kwa lengo la kuonja tamu na chungu yake. Namaanisha kuwa wakati mwingine mtu mbaya humfanya mwathirika awe na mapenzi mazuri kwa mpenzi wake anayefuata.
Unaweza kumchezea ‘faulo’ mwenzi wako. Ukawa kichwa ngumu hata pale anapokuwa anakuelekeza usahihi wa namna ya kuishi kimapenzi. Huyo anakuwa na kiburi kwa sababu hajawahi kukutana na mapenzi ya Jengua. Vuta kumbukumbu ya namna Jengua alivyokuwa anaishi na mke wake kwenye mchezo wa Kidedea.
Aina ya watu kama Jengua (yule wa kwenye maigizo) ni vizuri wakawepo kwa sababu wanasaidia kutoa masomo mazuri. Wengine ni kama Tomaso, eti kila kitu mpaka waone ndiyo waamini. Wanapotendwa, hukumbuka mambo matamu ya mpenzi aliyemletea kiburi.
Unakuwa kiburi kwa mwenzi wako, baada ya kuachana unakwenda kukutana na Jengua. Anakutenda inavyotakiwa mpaka unakoma. Sasa ndiyo unakumbuka yale yote uliyokuwa unamfanyia mpenzi aliyekupenda, kukujali na kukunyenyekea.
Mapenzi ni akili na utulivu. Usithubutu kuwa kama ndugu yangu Yohana, kwa tamaa yake ya kutaka kumiliki wanawake wawili, wakamuumiza kichwa. Walipogundua kichwa chake kimefeli, wakamchezesha sindimba. Ngoma inapigwa huku na kule hajui aende wapi.
Kama wanaambiana vile, mwanamke huyu analianzisha kivyake, eti anamhitaji haraka, mwingine naye anamtaka. Wote wanamfuata kijiweni, kila mmoja anataka aondoke naye. Yohana kajaziwa watu na wapenzi wake. Naye hajui aende wapi, akatae wapi.
Mwisho Yohana akawa mwendawazimu. Akipita barabarani anazungumza peke yake, wanawake wamemfanya awe mwehu. Hii siyo simulizi ya kufikirika, ni tukio ambalo lilimtokea ndugu yangu kwa tamaa ya kutaka kumiliki mabibi wawili kwa wakati mmoja.

No comments:

Post a Comment