Thursday, July 26, 2012

Ameshakuambia ana wake, unamng’ang’ania wa nini?

 MAPENZI ni sanaa yenye wigo mpana sana ndugu zangu. Unahitajika uwe mbunifu sana ili uweze kuendelea kuwa bora kwa mpenzi wako kila siku. Lazima uwe mtafutaji wa kitu kipya ili uweze kuwa wa tofauti kwa mwenzako.
Huwezi kuwa yuleyule, ikiwa hivyo maana yake utakinaiwa. Naam! Let’s Talk About Love ni safu nzuri kwako kwa ajili ya kuongeza maarifa na kukufanya uendelee kuwa bora zaidi kwa mpenzi wako.
Rafiki zangu, leo nataka kuzungumzia mada moja muhimu sana. Nazungumza na wale wenzangu ving’ang’anizi. Ni suala linalowasumbua wengi sana. Mtu anajua kabisa kwamba mtu anayemshawishi awe wake, tayari ana mpenzi wake, inakuwaje hapo?
Nimepata kesi nyingi sana za aina hiyo. Mwanamke anamtaka mwanaume ambaye ana mchumba wake au mume kabisa. Upande wa pili nao, mwanaume anamtaka mke wa mtu au mpenzi wa mtu. Maana yake ni nini sasa?
Mbaya zaidi, mwingine anaambiwa wazi kwamba ana mtu wake, lakini bado anang’ang’ania inasababishwa na nini? Haya ndiyo ambayo ninakwenda kuzungumza nanyi wapenzi wasomaji wangu.
VIPI MUME/MKE WA MTU?
Marafiki zangu asikudanganye mtu, mume/mke wa mtu sumu! Fanya ujanja wako uwezavyo, jifanye muhuni unavyoweza lakini si tabia njema kutoka na mtu ambaye ana mwenza wake (wengine wana ndoa kabisa).
Kwanza jiulize, kama ingekuwa ni wewe ungejisikiaje? Ukisia mkeo anatoka na mwanamke mwingine utajisikiaje? Au pengine umeolewa, halafu ukasikia au kupata uhakika kuwa mume wako anatoka na mwanamke mwingine utajisikiaje? Achana na hilo, unajiweka kwenye hatari kubwa, mwenye mali atakapogundua.

WENYE WAPENZI
Katika hali ya kawaida kabisa, unawezaje kumtaka mtu ambaye tayari unajua kuwa ana mtu wake? Busara hapo iko wapi? Ukijichunguza kwa makini lazima utagundua kwamba una tatizo.
Mtu ambaye tayari ana mpenzi wake, maana yake ni kwamba amefika; kitendo cha kumtongoza, kinaonesha ni kwa kiwango gani umejaa tamaa ambazo ndizo zinazokuongoza, maana kwa busara huwezi kumtaka mtu ambaye ana mpenzi wake.
Jambo la kushangaza zaidi ni kwamba, kuna wengine wanaambiwa wazi kuwa wana watu wao, lakini ndiyo kwanza mtu anaendelea kulazimisha, tena akitoa ahadi kedekede ili ampate. Huo ni ujinga usio na maana.

MAMBO YA KUJIFUNZA?
Kwa bahati mbaya, wanapokutana wote wa ‘hovyo’ wanajikuta wameingia kwenye mapenzi. Hebu jiulize wewe ambaye umeingilia penzi la mtu, akili yako inafanya kazi sawasawa kweli? Unawezaje kuingia kwa mtu ambaye tayari ana wake?
Kuna vitu kadhaa vya kujifunza hapa. Kwanza lazima utambue kuwa, huyo ambaye amekubali kuwa na wewe wakati huo huo ana mwingine, maana yake hana penzi la dhati. Si ajabu akiwa na wewe, akatafuta kuwa na mwingine pembeni yako!
Hekima iko wapi? Kuna tatizo gani kusubiri mwingine ambaye atakuwa wako peke yako? Tatizo wengi wanachukulia mapenzi kama maigizo tu. Hawaoni umuhimu wala thamani ya kupenda kwa penzi la kweli.
Lazima uwe na msimamo katika maisha yako. Siyo sifa kuwa na wapenzi wengi au kuingia kwenye uhusiano wa mwingine. Unadhani mwenzako anaumia kwa kiasi gani? Vipi kama na wewe ukija kuingiliwa na mtu mwingine?
Unahitaji kutulia na kuijua thamani yako, halafu kuacha tamaa ambazo hazina maana. Ni sifa njema kuwa na mwenzi wako peke yako bila kuchangia na mwingine. Hilo litawezekana kwako kama nawe utaacha tabia ya kuingia kwenye uhusiano wa wengine.

SHUGHULIKIA TATIZO LAKO
Tabia hiyo ni tatizo. Kama unayo unatakiwa ujue kwamba ni tatizo na unatakiwa kulishughulikia mapema iwezekanavyo. Mtu ambaye anaishi kwa kuongozwa na mapenzi ya kweli, hawezi kukubali kuwa na mtu ambaye ana mwenzi wake.
Kwa hakika utakuwa bado unaishi katika dunia inayotawaliwa na mawazo ya ngono tu. Ni dunia ya giza. Wenzako siku hizi wanatafuta kuishi kwenye ulimwengu wa mapenzi ya kweli. Ondoka kwenye hilo giza. Hayo mambo yalikuwa ya kizamani sana, siyo katika zama hizi tulizaonazo.

No comments:

Post a Comment