Thursday, January 10, 2013

WACHINA WAZUIA UPANUZI WA BANDARI YA DAR

 
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.  

* Waziri Dk. Mwakyembe, Jaji Werema wageuziwa kibao,washitakiwa
WIKI hii kona ya Fumuafumua ilizama bandarini Dar es Salaam na kugundua kuwa shughuli za upanuzi wa bandari kama serikali ilivyokusudia imekwama na kuwa ni ndoto kwa wakati huu.
 
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Hata hivyo, katika dodosadodosa yetu tumegundua kuwa kuna kesi ambayo imefunguliwa na imezuia muendelezo wowote wa upanuzi wa bandari hiyo ili iwe ya kisasa zaidi.
Imegundulika pia kuwa Kampuni moja ya Kichina iitwayo China Communications and Constraction (CCC) ndiyo iliyoenda Mahakama Kuu, kitengo cha biashara na kuzuia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutangaza zabuni ya upanuzi wa bandari hiyo.


Kampuni hiyo imefanya hivyo kufuatia mgogoro kati yake na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na ikadai mahakamani kwamba imesikia kuwa mdaiwa wao anataka kutangaza zabuni ya upanuzi wakati walishaingia mkataba na tayari wameshatumia gharama kadhaa.
Kampuni hiyo inaitaka mahakama kuzuia zoezi hilo hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba maombi hayo yamekubaliwa na mahakamani kuu katika kitengo hicho cha biashara.
Kampuni hiyo chini ya wakili wao Richard Rweyongeza, imefungua shauri la maombi hayo dhidi ya TPA, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Uchunguzi zaidi umebaini kwamba Desemba 31, mwaka jana ndipo ombi hilo lilipotajwa mbele ya Jaji Agness Bukuku huku kesi ya msingi ya kupinga kunyang’anywa zabuni hiyo bila fidia ikipangwa kuanza kusikilizwa Januari 28, mwaka huu mahakama hapo.
Tayari TPA imekwama kufanya lolote kuhusiana na upanuzi wa bandari hiyo baada ya mahakama kuiamuru Serikali ya Tanzania kutofanya lolote katika mchakato wa zabuni ya upanuzi wa bandari hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Kampuni hiyo iliingia mkataba wa kufanya upembuzi yakinifu wa upanuzi wa bandari hiyo na inadai imeshatumia dola za Kimarekani 500,000 (zaidi ya shilingi milioni 750) katika maandalizi ya awali ya mradi huo.
Habari za kimahakama zinasema katika shauri hilo TPA inawakilishwa na Wakili Peter Kibatala.

No comments:

Post a Comment