Baada ya wanawake kwa miaka mingi kuwa ndio wenye jukumu la kutumia
vidonge na njia nyingine katika kupangilia uzazi, watafiti nchini China
wamekamilisha utafiti wao ambao utawasaidia wanaume kuwasaidia wanawake
jukumu hilo baada ya kutoa sindano kwaajili ya wanaume zitakazosimamisha
uzalishaji wa mbegu za kiume kwa muda Wanasayansi nchini China
wamekamilisha utafiti wao wa sindano kwaajili ya wanaume ili kusaidia
kuzuia mimba zisizohitajika.
Sindano hizo zinasimamisha kwa muda uzalishaji wa mbegu za kiume na
watafiti hao walisema kwamba uzalishaji wa mbegu za kiume unaweza
ukaendelezwa muda wowote ule.
Watafiti hao waliwatoa wasiwasi wanaume kwa kusema kuwa hakuna madhara yoyote yanayotokana na matumizi ya sindano hizo.
Kwa miaka mingi wanawake wamekuwa wakitumia vidonge na njia nyingine
mbali mbali za kuzuia mimba zisizohitajika huku wanaume wakibakia na
chaguo moja tu ambalo ni matumizi ya kondomu au kufunga kizazi kabisa
kwa njia ya vasektomi.
Wanaume 1,000 wa nchini China wenye umri kati ya miaka 20 na 45 ambao
kila mmoja wao alikuwa tayari ana mtoto mmoja au zaidi walishirikishwa
kwenye majaribio ya sindano hizo kwa kuchomwa sindano hizo kila mwezi
kwa muda wa miezi 30 mfululizo.
Majaribio hayo yalionyesha mafanikio makubwa kwani katika watu 1,000 ni
mtu mmoja tu ndiye aliyefanikiwa kumpa ujauzito mpenzi wake wakati
akiendelea na sindano hizo.
Mwisho wa utafiti huo, mfumo za uzazi wa wanaume wote walioshiriki
kwenye utafiti huo ulirudi katika hali yake ya kawaida isipokuwa wanaume
wawili tu.Wanasayansi wamesema watautumia utaalamu uliotumika kujaribu
kutengeneza vidonge vitakavyotumiwa na wanaume kusaidia kuzuia mimba
zisizohitajika.
Hata hivyo wanasayansi hao walikumbusha kwamba matumizi ya sindano hizo
hayamaanishi kwamba ndiyo yatakuwa kinga ya magonjwa ya zinaa.
"Tunawahimiza watu watumie kondomu ili kujikinga na magonjwa ya zinaa" walisema watafiti hao.
No comments:
Post a Comment