Thursday, July 19, 2012

MBINU 13 ZA KUYAVUKA MAISHA YA HUZUNI


TUANZE kwa kutafakari baadhi ya taarifa za kuhuzunisha, ambazo wengi wetu tunakutana nazo kila siku katika maisha yetu. “Kuanzia leo umefukuzwa kazi”, “Nimeamua tuachane”, “Baba yako mzazi amefariki leo asubuhi”,  “Mwanao amefariki.” Bila shaka taarifa za aina hii zinahuzunisha na swali linabaki tufanyeje tunapokuwa na mawazo ya aina hii?
Ukweli ni kwamba, yakitokea mawazo mabaya katikati ya furaha huwezi kuiondoa, lakini pamoja na hayo baadhi ya watu hutumia muda mwingi sana kuhuzunishwa na tatizo ambalo pengine lingeweza kumalizwa kwa saa chache na mhusika kubaki huru.
      Wapo watu kati yetu wanaweza kufuga mawazo ya kuachwa na wapenzi wao kwa miaka mitano mfululizo, huku wengine wakitumia miezi mingi kuondokana na huzuni iliyotokana na kutukanwa na wazazi, kufokewa na bosi, kupata hasara katika biashara,   kufeli mitihani na kadhalika.

Hii ina maana kuwa ni wachache kati yetu tunaofahamu namna ya kupambana na mawazo yanayohuzunisha na kuyashinda. Kwa kuzingatia umuhimu wa kutunza furaha yetu katika maisha, nimeona ni vema nikawafundisha hatua za kuondokana na mawazo yanayoumiza yatokanayo na matukio ya kuhuzunisha.

KWANZA: Mtu anapojikuta katika mawazo ya kuhuzunisha lazima, aanze kwa kurekebisha kwanza mhemko wake kwa kushughulikia mfumo wa upumuaji. Unapoletewa taarifa mbaya, moyo hushtuka na kuufanya uende mbio, hivyo ili kuurudisha katika hali yake ya kawaida unatakiwa kuvuta pumzi kwa wingi ndani na kuzitoa nje pole pole. Hatua hii itasaidia kurudisha mapigo ya moyo katika hali yake ya kawaida.

PILI: Baada ya zoezi hilo, mwenye mawazo ya kuumiza anatakiwa kujilazimisha kutabasamu mara kwa mara, hata kama hawezi kufanya hivyo kwa wakati huo kutokana na tukio lililomletea mawazo mabaya. Kutabasamu husaidia kuchangamsha akili, ingawa inaweza kuchukua muda kurudi katika hali ya kawaida, lakini wataalamu wanasema inasaidia kuamsha hisia za furaha zilizokuwa zimeshambuliwa na mawazo mabaya.

TATU: Katika hali ya kawaida uvamizi wa mawazo mabaya unapotokea hukuta mawazo mengine yakiwemo akilini na kuyaondoa, kisha yenyewe kuchukua hatua za kutawala akili, unashauriwa baada ya kutekwa na mawazo hayo chukua hatua ya kujilazimisha kurudisha akilini mawazo yaliyokuwemo awali kabla hujavamiwa. Lengo ni kutafuta nafuu na kufufua mawazo yenye kufurahisha.

NNE: Ikiwa wewe mwenyewe huwezi kufurahi baada ya kuchukua hatua hizo, wasaidie wengine waliopo karibu yako kufurahi.
Kwa mfano unapokuwa kwenye msiba unalia, chukua jukumu la kuwanyamazisha wenzako na kuwapa faraja. “Nyamazeni, kazi ya Mungu haina makosa” ukifanya hivyo utakuwa umejisaidia wewe pia kuondokana na mawazo ya msiba yaliyokufanya ulie sana.


TANO: Watu wengi wanapokuwa na mawazo ya kuumiza huwa wanadhani kuwa jukumu la huruma liko mikononi mwa watu wengine. “Tangu nimepata msiba, kaka yangu hajafika hata kunipa pole.”
Mawazo ya aina hii yakiongezwa kichwani huzuni huwa mara dufu, hivyo ni jukumu la mhusika kujihurumia mwenyewe na kujiuliza mwisho wa huzuni isiyokoma ni nini kama si kifo chake?

SITA: Baada ya kupoteza furaha, jambo jingine muhimu ni kuujali mwili wako kwa kula chakula kizuri, kunywa maji na kujitibu kama mawazo yako yameacha maumivu ya kichwa au mwili! Lakini jambo la kushangaza watu wengi wanapokuwa na mawazo hususa hata kula, jambo ambalo hudhoofisha afya zao na kuwaongezea matatizo zaidi.

SABA: Namna nyingine ya kukabiliana na mawazo ya kuumiza ni kupunguza hasira juu ya watu wengine. Katika hali ya kawaida matukio mengi husababishwa na watu, kumkasirikia mtu aliyekusaliti, aliyekufilisi, anayekuroga ni adhabu nyingine kubwa unayojipa mwenyewe, vema ukawa mtu wa kusamehe.

NANE: Unapokuwa na mawazo yanayoumiza na baadaye ukafanikiwa kuyaacha usikubali kuyarudia tena, lakini watu wengi wanaoumizwa na mambo fulani huwa hodari sana kuyatunza akilini mwao na kuyarejea kila mara, jambo ambalo huwafanya waumizwe na mawazo hayo kwa muda mrefu bila kupumzika. Yametokea, yamepita achana nayo usikubali akili yako iyarejee tena.

TISA: Ikiwa umekuwa na mawazo ya kuumiza kwa muda mrefu, kwa sababu umefeli mtihani au umeshindwa kufanya jambo fulani, mtu kakuudhi, hebu badili mawazo hayo ya kushindwa na ufikirie kushinda katika siku za usoni.

KUMI: Yapo baadhi ya mambo ya kuhuzunisha ambayo hutukumba bila kutarajia na hivyo kutuletea mawazo. Njia pekee ya kuyaepuka mawazo ya aina hii ni pamoja na kukubali tukio husika.
Wengi wetu tunapofiwa kwa mfano huwa hatukubali kuamini kilichotokea, matokeo yake ni kuumia kwa muda mrefu. Unapokuwa na tatizo, kwanza likubali kisha chukua hatuza za kulikabili.

KUMI NA MOJA: Msongo wa mawazo unapokuvamia unatakiwa wakati mwingine uchukue hatua za kujipumzisha sehemu tulivu, likiwepo suala la kulala kama inawezekana. Hatua hii itasaidia kuupumzisha mwili na akili kiasi cha kuufanya upate nguvu ya kukabiliana na tatizo.
Hushauriwi kuchukua hatua unapokuwa na msongo mkali wa mawazo. Kama mtu amekuudhi, achana naye nenda kajipumzishe, kesho utajikuta umepata nguvu ya kumpuuza na kuachana naye kabisa.

KUMI NA MBILI:
Wakati mwingine kujua sababu zilizoleta tatizo ni muhimu na kwamba hupunguza msongo wa mawazo. Hivyo unapokuwa na jambo ambalo linaikera akili yako, jaribu kutafuta chanzo chake, inawezekana taarifa zinazokuumiza zikawa si sahihi.

KUMI NA TATU:
Watu wengi wanapopata matatizo ambayo huwatumbukiza katika mawazo mabaya huwa hawako tayari kulipa gharama za kuyamaliza, matokeo yake hubaki wakihuzunika. Kwa mfano, mtu anadaiwa, mdai wake akamfuata na kumtolea lugha za matusi, jambo la ajabu mdaiwa badala ya kujituma kuhakikisha analipa deni ili ajikomboe anabaki kuhuzunikia matusi. Unapokuwa na tatizo jitume kulimaliza.

No comments:

Post a Comment