Kuna
tofauti kubwa ya kimaamuzi kati ya mwanaume na mwanamke kwenye suala la
kuachana. Inaelezwa kwamba, wanaume ni rahisi kwao kuamua ndani ya
dakika moja na kutangaza kuvunja uhusiano, lakini kwa wanawake maamuzi
yao mara nyingi hutanguliwa na dalili, ingawa hata wanaume nao wanazo.
Uchunguzi
unaonesha kuwa, wanawake wengi hawawezi kuficha sana hisia zao za
mapenzi, lakini pia kwenye chuki hawakujaaliwa uvumilivu. Wanasaikolojia
wanakiri kwamba, kutambua mawazo yaliyomo ndani ya mwanamke kwa
kumtazama muonekano wake usoni ni rahisi kuliko mwanaume ambaye anatajwa
kuwa na uwezo kuficha mawazo yake.
Muongozo huo wa kitaalamu wa
kumtambua mwanamke anayekaribia kukuacha ni kazi rahisi, ambayo inaweza
kuanzia kwenye kona ya mazoea ya tabia zake za kila siku kwenye uhusiano
wa kimapenzi. Ni imani yangu kuwa kila mwanaume anamfahamu mpenzi wake
katika sura mbili za chuki na furaha yake.
Atakuwa mwanaume wa
ajabu ambaye atarudi nyumbani kwake na kushindwa kusoma sura ya mkewe na
kujua kama ana furaha au amekwazika.
Ninapotazama uwezekano rahisi
wa kumtambua mwanamke, nafika mahali pa kuamini kuwa dokezo chache
nitakazotoa hapa chini zinaweza kuwa msaada kwa wanaume wengi kujua kama
wamekaribia kuwekwa kando kimapenzi.
KUPENDA KUJITENGA
Mwanamke
ambaye anapenda kujitenga na mpenzi wake atakuwa kwenye hatua za awali
za kuelekea kuachana naye. Tabia ya mwanamke kutopenda kukaa karibu na
mumewe au mpenzi wake inatajwa kama ishara ya kuchoka au kukinai penzi.
Hoja inabaki pale niliposema pa yeye kushindwa kuamua haraka na hivyo
kutengeneza kwanza hali ya kumpuuza mpenzi wake.
KUPOTEZA HAMU YA TENDO
Mwanamke
ambaye hafurahii tendo la ndoa kwa mumewe au mpenzi wake yuko kwenye
hatua za kuacha. Mara zote msisimko wa kimapenzi huashiria utoshelevu wa
kihisia ambao ndiyo unaoelezwa kuwa ni muhimu kwenye uhusiano wa
kimapenzi kuliko kitu kingine chochote.
Hii ina maana kwamba,
mwanamke anayetosheka na kuvutiwa na mwanaume aliyenaye hawezi kukosa
hisia za kimapenzi hasa anapokuwa na mwenza wake faragha.
KUPENDA KUKOSOA
Kama
nilivyosema, kujua historia ya penzi lenu namna lilivyoanza ni jambo
muhimu kwa sababu husaidia kujua kama kuna mabadiliko hatari ya tabia za
mwanamke.
Ikitokea mpenzi wako ambaye hapo mwanzo alikuwa msikivu
na ghafla ukaanza kuona amekuwa mkosaji na mpingaji wa mwenendo wako au
kila unachofikiria kukifanya, tambua kuwa hiyo ni ishara kuwa amechoka
kilichobaki ni nafasi ya kukuacha.
UHUSIANO NA MTU MWINGINE
Licha
ya kwamba usaliti kwenye uhusiano limekuwa suala la kawaida siku hizi,
lakini mwanamke ambaye atakuwa hafichi uhusiano wake wa pembeni na
kuacha minong’ono ikikufikia huku yeye akionesha kutojali malalamiko
yako ya kusalitiwa, ujue hiyo ni ishara kwamba mwanaume wa pembeni
amemfikisha kwenye hitaji la moyo wake na hivyo kuachana na wewe si
jambo la gharama kwake.
KUTOKUKUTEGEMEA
Mwanamke ambaye ana
kusudio la kukuacha huanza kwa kuuondoa utegemezi. Ikiwa alikuwa
anakuomba nauli, fedha ya matumizi, ada na huduma nyingine atasitisha
bila kukuambia na bado utaona anaendelea kujimudu kama kawaida au
kuteseka kimya kimya. Kuacha kukutegemea kama zamani ni dalili za kuweza
kuishi bila wewe na hivyo kutafsiri uwezekano wa kukuacha wakati
wowote.
No comments:
Post a Comment